TP MAZEMBE YAKOMALIA SAINI YA FEI TOTO YANGA
MABINGWA mara 5 wa Bara la Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamedhamiria kuinasa saini ya nyota wa Klabu ya Yanga SC, Feisal Salum ‘Fei Toto’. Taarifa kutoka jijini Lubumbashi zimeeleza juu ya klabu hiyo kumtaka kiungo wa Yanga SC.
Klabu ya TP Mazembe imetenga dola za Kimarekani laki 2 ambazo ni zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 460 ili kuinasa saini ya Fei Toto. Klabu ya TP Mazembe ambao pia ni mabingwa wa ligi kuu ya soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maarufu kama Linafoot, wanamhitaji Fei Toto ili kuziba pengo lililoachwa na mchezaji wao Isaac Tshibangu.
Mchezaji Isaac Tshibangu aliachana na matajiri wa Lubumbashi, klabu ya TP Mazembe na kuamua kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Anderlecht ya nchini Ubelgiji.
Kwa mantiki hiyo, Rais wa klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi Chapwa, anafanya kila jitihada ili kuweza kupata mbadala wa mchezaji huyo.
Endapo dili hilo litakamilika, mchezaji Feisal Salum Abdallah ” Fei Toto” , atafuata nyayo za wachezaji wengine wa kitanzania waliowahi kusajiliwa na kukipiga katika klabu hiyo. Wachezaji wachache wa Kitanzania waliowahi kucheza katika klabu ya TP Mazembe ni pamoja na; Mbwana Ally Samatta, Thomas Ulimwengu, Eliud Ambokile na Ramadhani Singano maarufu pia kwa jina la ‘ Messi’ .
Awali iliripotiwa kuwa, klabu ya Yanga SC itaenda kuweka kambi katika jiji la Istanbul nchini Uturuki! kwa sasa, klabu hiyo inadaiwa kubadili uelekeo na sasa inadhamiria kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa mashindano katika taifa la Afrika Kaskazini la Morocco.
Kambi hiyo ya Yanga SC, inatarajiwa kuanza mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya CECAFA Kagame Cup. Wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza cha Yanga SC, watapewa wiki 2 za kupumzika kabla ya kurejea tena kambini kujiunga na wale wapya waliosajiliwa na watakaoshiriki Kagame Cup.
Baada ya muunganiko wa kikosi kizima cha Yanga kukamilika, safari ya Yanga SC kwenda kuweka kambi nchini Morocco itaanza rasmi.
No comments