Jeuri ya pesa… Mo, Ghalib waonyesha ubabe!
MABILIONEA wawili wazito kwenye soka la Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ na Ghalib Mohammed wametoa kauli ambazo zitaamua kwa asilimia 90 mechi ya Jumapili mjini hapa.
Mo ambaye muwekezaji wa Simba, alikutana na mastaa wa Simba jana Jijini Dar es Salaam na kuwaahidi mkwanja na furaha kubwa kisha wakaondoka na mzuka wa aina yake kuelekea Uwanja wa Ndege na wakatua hapa jioni.
Yanga nao, Ghalib ambauye ni mdhamini kupitia GSM amekutana nao kambini na mazoezini na kwa nyakati tofauti wiki hii na kuwaahidi kwamba wakifanya mambo tena Jumapili, watakumbana na mkwanja mzito kuliko ule wa mechi ya bao 1-0 Jijini Dar es Salaam. Kumbuka Jumatatu wiki hii Yanga wakitokea Dodoma waliingiziwa sio chini ya Sh19 milioni kila mchezaji kama bonasi ya kuwapiga Simba.
Sasa Mo kaweka mzigo, Ghalib kaweka mzigo. Kigoma patachimbika kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
Msimbazi mabosi wa Simba wamewajaza upepo nyota wao kwa kuwatangazia dau la zaidi ya Sh250milioni kama watawapiga watani wao ambao wametua jana asubuhi kwa mbwembwe nyingi mjini hapa.
Mmoja wa viongozi wa Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa fedha hizo zitatokana na ahadi ya Mo, bonasi na zawadi za ubingwa kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadhamini Azam Media.
Kiasi cha Sh 50 milioni ni fedha ambayo bingwa wa mashindano hayo anapata kama zawadi na inayobakia itakuwa ni bonasi kutoka kwa uongozi kama ambavyo umekuwa ukifanya katika mechi kubwa.
“Suala la bonasi kwetu ni la kawaida na safari hii tumepanga fedha yote ya ubingwa ambayo inatolewa kama zawadi watapewa wachezaji lakini pia kuna fedha ambayo uongozi tumekuwa na kawaida ya kuwapa wachezaji kama bonasi kila tunaposhinda mechi ya watani na kwenye mashindano ya kimataifa.
Mara nyingi bonasi yetu huwa inaanzia kiasi cha Sh 200 na inaweza kuzidi hivyo kazi kwao wachezaji lakini sisi kwa upande wetu uongozi tunajitahidi kuhakikisha wanakuwa vizuri kuelekea mechi hiyo,” alisema kigogo huyo.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema; “Maandalizi kwa upande wetu yanaendelea vizuri na uongozi akili yetu tunaielekeza katika mchezo huo.”
Kocha wa Simba, Didier Gomes, alisema Simba itashinda mechi hiyo kwa ajili ya mmiliki Mo Dewji, mashabiki na Barbara, ambaye tangu juzi usiku alijikuta katika mzozo na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na kiu ya kulitwaa taji la mashindano hayo kwa mara ya pili mfululizo lakini pia kulipa kisasi cha kupoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.
Ilianza kwa kufungwa kwa mikwaju ya penati 4-3 kwenye Fainali ya Kombe la Mapinduzi na ikaja kupoteza kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu.
YANGA NAKO
Mwanaspoti linajua kwamba bilionea Ghalib Said Mohammed ambaye ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga amewaambia wachezaji kambini kwamba wakiipiga Simba atatoa zaidi ya Sh500milioni alizowapa kwenye mechi iliyopita.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga aliidokezea Mwanaspoti kwamba amewasisitiza wachezaji wamfurahishe na yeye atawafurahisha zaidi ya ilivyokuwa mara ya mwisho.
“Amekuwa na ahadi za uhakika na ametuongezea morali wachezaji wote kuanzia kambini, uwanja wa mazoezi na hata siku yenyewe ya mechi,” alisema mchezaji huyo na kuongeza;
“Kama katika mechi iliyopita baada ya kuwafunga Simba mchezaji mmoja aliyecheza tu alipata si chini ya Sh20 milioni sasa safari hii pesa hiyo inazidi tutaenda kupambana mpaka mwisho kuona tunashinda tena mbali ya faida nyingine kama kuchukua kombe, kuwafunga Simba na mengineyo mengi.”
YANGA WAMKATAA REFA wa fainali
Kupitia barua yao rasmi, Yanga jana waliitaka TFF kutafakari uamuzi wa kumpa refa Ahmed Arajiga mechi zilizofuatana za Simba kuanzia robo fainali, nusu fainali na fainali za msimu huu.
“Uongozi wa Yanga unaamini Tanzania ina waamuzi wengi wenye uwezo, hivyo kitendo cha kumrudia mwamuzi mmoja katika mechi tatu za timu moja katika shindano moja kinatisha shaka,” ilisomeka barua hiyo ya rangi ya njano.
SAPRAIZI KIGOMA
Viongozi wa Yanga jana walifanya umafia kwa kutua kwa kushtukiza jijini hapa. Walitua mapema asubuhi huku mamlaka za soka, ulinzi na wadau wao wengine wakiwatarajia kuwasili mchana wa jua kali kwa ndege.
Lakini mmoja wa viongozi aliiambia Mwanaspoti kwamba waliamua kutua kwa muda tofauti na waliokuwa wameripoti kutokana na sababu binafsi ambazo ni kama mbinu za kiutani wa jadi. “Hizi ni mechi kubwa na zina mbinu nyingi za ndani na nje ya uwanja, lazima saa nyingine ufanye mambo ambayo unaona wewe ni sahihi, haswa ukizingatia kwamba sisi na Simba tunajuana,” alidokeza kiongozi mmoja wa Yanga kwenye msafara huo uliokuwa ukitegemewa kuwasili saa 9 alasiri.
Imeandikwa na Happy tesha, Thobias Sebastian na Clezencia Tryphone
No comments