Breaking News

Nini maana ya mwisho wa Uenyekiti wa Mbowe Chadema?




Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ametangaza kutogombea uenyekiti wa chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2023 ingawa tangazo hilo lililotolewa pasi na mbwembwe za namna yoyote, licha ya kuwa mwangwi wake ni mkubwa katika siasa za Tanzania.

Mbowe, pengine kuliko mwanasiasa mwingine yeyote wa upinzani nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ameshiriki katika kutengeneza aina ya siasa za upinzani zilizopo nchini kwa sasa.

Amekuwa kiongozi wa upinzani nchini chini ya marais wanne tofauti kutoka chama tawala cha CCM na mara zote ametumia fursa na changamoto za wakati husika kukijenga chama chake na kujihami dhidi ya wapinzani wake ndani ya chama hicho.

Tangazo hili la Mbowe linamaanisha kwamba katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Chadema itahitaji kuwa na Mwenyekiti mpya kwa ajili ya kukipitisha katika nyakati zijazo na kumalizia zama za kipekee katika siasa za Tanzania.

Ukuu wa Mbowe ndani ya Chadema


Wakati anakabidhiwa kuongoza chama mwanzoni mwa miaka ya 2000, Chadema kilikuwa chama cha upinzani cha kibwanyenye kinachofuata siasa za mrengo wa katikati kulia na chenye wabunge wanne katika Bunge la Tanzania.

Katika kilele cha mafanikio ya Chadema, chama hicho kilifikia mafanikio ya kuwa na zaidi ya wabunge 100 ndani ya Bunge na kutengeneza mtandao wa wanachama na wafuasi karibu katika kona zote za Tanzania.

Kwa sasa, hakuna mahali hapa nchini ambako unaweza kusema chama hicho hakijafika.

Kuna mambo makubwa kama manne ambayo Mbowe aliyafanya wakati wa zama zake za uenyekiti yaliyosaidia kuifikisha Chadema ilipo sasa.

Mambo hayo ni mchanganyiko wa bahati, mbinu za kimkakati, uwezo wa kifedha na kuwa na watu wenye akili na maarifa.

Jambo la kwanza alilolifanya Mbowe lilikuwa ni kuamini katika vijana. Vijana walikuwa sehemu ya harakati za kudai mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania lakini ni Mbowe ndiye aliyekuwa tayari kuwatafuta na kuwapa nafasi kubwa za uongozi vijana na kutoa picha kwamba chama hicho ni cha vijana.

Katika taifa ambalo zaidi ya nusu ya wananchi wake wamezaliwa baada ya mwaka 1999, suala hili lilikuwa ni kete muhimu kisiasa kwa sababu vijana ndiyo wanaotengeneza kundi kubwa la Watanzania.

Vijana waliokuja kutikisa katika siasa za Tanzania kama vile Zitto Kabwe, John Mnyika, Halima Mdee, John Mrema na wengineo wengi walionwa mapema na kutongozwa na Mbowe ambaye pia alichukua jukumu la kuwalea kisiasa.

Kwa sababu alivuna vijana hao kutoka kada ya kitaaluma, Mbowe alifanikiwa kujenga kada ya wanasiasa vijana wenye upeo mkubwa wa mambo, wanazoungumza kwa kujiamini na uwezo mkubwa wa kujenga hoja. Baada ya mafanikio ya wabunge vijana wa Chadema wa Bunge la mwaka 2005-2010, vijana wengi waliamua kujiunga na chama hicho wakifahamu kuna fursa ya kutumika ipasavyo.

Mbowe pia alikuwa na bahati kwamba uenyekiti wake ulijikita katika wakati ambapo Tanzania iliongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliamini katika mfumo wa demokrasia ya vyama na kuachia Bunge la Tisa lililoongozwa na Samuel Sitta kutoa nafasi kwa wabunge kuihoji na kuisimamia serikali ipasavyo.

Matukio yaliyotokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, yamewafundisha Watanzania kwamba endapo Rais wa Tanzania katika kipindi cha kati ya 2005-2010 angekuwa hayati John Magufuli, huenda Chadema isingepata nguvu na mafanikio iliyoyapata wakati wa utawala wa Kikwete.

Jambo lingine ambalo Chadema ilikuwa nalo na vyama vingine havikuwa navyo ni kuwa na hazina ya viongozi wa zamani wa serikali wa kiwango cha Edwin Mtei na hayati Bob Makani lakini wakati huohuo ikiwa na wasomi wa kiwango cha Dk. Wilbrod Slaa, Profesa Mwesiga Baregu, Mabere Marando, Profesa Kitila Mkumbo na Kabwe.

Matokeo yake ikawa kwamba vikao vya Chadema vilikuwa ni chemchem ya mijadala mikali ya hoja na uvumbuzi wa ajenda muhimu kwa ajili ya kujiongezea wafuasi. Muda si mrefu, Chadema kilijitambulisha kama chama chenye ajenda sahihi na maono safi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Chadema ilikuwa na bahati pia ya kuwa na watu kama Mbowe mwenyewe, hayati Philemon Ndesamburo, Mtei na watu wengine wasiojulikana waliokuwa tayari kuingia mifukoni mwao na kujitolea kifedha kuendesha Chadema.


Kwa sababu hiyo, wakati akili za ndani ya chama zilipopendekeza matumizi ya helikopta kwenye kampeni, Chadema ilikuwa na watu waliokuwa tayari kufadhili matumizi ya usafiri huo ikiwa ni mara ya kwanza katika siasa za Tanzania.

Wakati chama kikiamua kuanza Operesheni Sangara ya kukitangaza chama katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, chama kilikuwa na uwezo wa kufadhili ziara nzima.

Mbowe ni mbobezi katika kupanga mipango ya kukitangaza chama chake.

Ni katika wakati wake ndipo Chadema ilipoanza kutumia helikopta katika kampeni zake ikitumia muda mfupi kuwafikia Watanzania katika maeneo ambako barabara zilikuwa taabu, akaibuka na vazi kama la kombati lililokuja kuwa mojawapo ya alama za Chadema na chama hicho kikajenga uwezo mzuri wa kujenga majukwaa mazuri kwa shughuli za kisiasa.

Ikawa mikutano ya Chadema inahudhuriwa hata na watu wa vyama vingine kwa sababu ya hoja za wazungumzaji, umahiri wa jukwaa, kuona helikopta na sauti nzuri kutoka kwenye majukwaa.

Mwaka 2010, chini ya Mbowe tena, Chadema ilifanya jambo lililowashtua hadi waasisi wake. Aliyekuwa mgombea urais wake, Dk. Slaa alifanya kampeni za kipekee akiahidi Watanzania huduma bure za afya na elimu.

Misingi ya uanzishwaji wa Chadema ilikuwa ni ubepari na mambo kama ya elimu bure ni kinyume na misingi hiyo. Ilibidi kwanza Mbowe awakubalie akina Slaa, Kitila, Baregu na Zitto waliotaka sera hizo wakiamini zina mashiko kwa Watanzania na kisha ajipe kazi ya kuwashawishi wazee waasisi kwamba Chadema bado ni ileile.

Mwaka 2015, Mbowe tena alifanikiwa kushawishi wanachama wa Chadema kumpokea na hatimaye kumpitisha Edward Lowassa aliyehamia kutoka CCM awe mgombea urais wake.

Matukio hayo muhimu katika uongozi wa Mbowe yanamuonyesha kama kiongozi mbunifu, anayeamini vijana, asiye mhafidhina wa kisera na mwenye uwezo wa kufanya kazi na yeyote kwa maslahi ya chama chake.



No comments