Breaking News

Yoweri Museveni: Kipi cha kutarajia akianza miaka mitano mingine madarakani Uganda?

 



Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 kwa mapinduzi ya kijeshi.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 kwa mapinduzi ya kijeshi.

Leo Mei 12, 2021 Rais Yoweri Museveni anatarajiwa kuapishwa kuendelea kuiongoza Uganda. Ikulu ya rais iliarifu wiki iliyopita kuwa wakuu wa nchi kumi na moja wamethibitisha kuhudhuria hafla hiyo.

Museveni ataiongoza Uganda kwa miaka mengine mitano, ikiwa ni muhula wake wa sita madarakani. Aliingia madarakani Januari 1986 kwa mapinduzi ya kijeshi, hadi utakapofika uchaguzi mwingine 2026 atakuwa madarakani kwa miaka 40, sawa na miongo minne. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 81.

Yupo katika kundi moja na Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang, Rais wa Cameroon Paul Biya, Rais wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville) Denis Sassou Nguesso, na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki.

Ni orodha ya Marais wakongwe barani Afrika ambao hadi sasa bado wapo madarakani. Kwa Afrika Mashariki Museveni anashika bendera kwa kuwa mtawala wa muda mrefu juu ya kiti chake.


Alishinda uchaguzi wa Januari 14, 2021 kwa kuwabwaga wagombea wengine kumi katika nafasi ya Urais kwa ushindi wa asilimia 58 ya kura zote. Mbio za Robert Kyagulanyi kwa lakabu ya za Bobi Wine kumtoa madarakani, zimeenda kapa. Japo wapinzani nchini humo pamoja na waangalizi wa kimataifa na makundi ya haki za binaadamu kudai kuwa uchaguzi huo uliingiliwa na serikali ya Museveni na kuminya wagombea wa upinzani. Madai hayo hata hivyo yanakanushwa na serikali.

Ana nguvu gani kisiasa na kiusalama?

Chini ya chama chake cha National Resistance Movement (NRM), Museveni ana nguvu za kisiasa. Chama hicho kimeshinda wingi wa viti vya Ubunge katika Bunge la tisa, licha ya kushindwa katika baadhi ya ngome zake na chama cha NUP.

Uganda haijawahi kushuhudia ubadilishaji wa madaraka kwa njia ya amani. Tangu wakati wa Marais waliopita Edward Mutesa, Milton Obote, Idd Ami, Yusuf Lule, Godfrey Binaisa, Paulo Muwanga, Bazilio Olara Okello, Generali Tito Okello na sasa Museveni.

Wafuasi wa Museveni wanaamini bado ana mengi ya kuifanyia Uganda hata baada ya kukaa madarakani kwa miaka 35.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa Museveni wanaamini bado ana mengi ya kuifanyia Uganda hata baada ya kukaa madarakani kwa miaka 35.

Mambo yamekuwa ya mwenye nguvu mpishe. Taifa hilo limepita katika tawala za kijeshi na kiraia, mapinduzi, vita na machafuko. Baadhi ya watawala hao majina yao siyo maarufu kwa sababu hata mwaka haukutimia vyema waliondoshwa madarakani.

Ambalo Museveni amewashinda watangulizi wake ni kuweza kudumu muda mrefu na kuiweka nchi katika amani na kuinusuru na migogoro ya kisiasa na kikabila. Hujitapa kwa mafanikio hayo, kwa kusema Uganda haiendeshi tena siasa kwa sera za dini na makabila.

Bahati mbaya, mafanikio hayo yamekuja na gharama yake. Ambayo ni kukandamiza demokrasia na kutumia vibaya vyombo vya usalama. Ukandamizaji huo ni kama chakula kinachomfanya azidi kunenepa na kuongeza nguvu.


Nguvu zake haziishii hapo. Chama chake cha NRM kina ushawishi mkubwa katika vyombo vya usalama. Ushawishi huo ndio unaomuhakikishia kuendelea kuwa hai madarakani bila misukosuko kama watangulizi wake.

Disemba 2020, mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu. Rais Museveni alimteua mwanawe wa kiume, Luteni Jenerali Muhoozi Kaine-rugaba kuwa kamanda wa kikosi maalum cha ulinzi wa Rais.

Muhoozi ana uzoefu mkubwa na shughuli za kiusalama. Amewahi kuhudumu nchini Somalia katika kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM kulinda amani. Uteuzi wake yumkini ni hesabu za Museveni kujihakikishia usalama wakati taifa likiingia katika uchaguzi.

Nguvu zake kisiasa zitaendelea kuwepo ndani ya miaka mengine mitano ya uongozi wake. Ingawa baada ya kutimiza miaka 81 kutakuwa na kitendawili ikiwa ataingia katika uchaguzi tena au atapumzika ama atapumzishwa.

Nguvu alizonazo atazitumia kuendelea kuituliza nchi. Kwa upande mwingine atazitumia kupambana na wapinzani wake kisiasa. Kwa hakika anajua vyema kucheza karata ya kuendelea kubaki madarakani bila kitisho chochote.

Demokrasia na Uchumi

"Hatutonyamazishwa, Museveni anapaswa kuondoka." Ndivyo linavyosomeka moja ya makumi ya mabango kutoka kwa wafuasi wa Bobi Wine walioandama nchini Uingereza, Ijumaa ya tarehe Mei 8, 2021.

Maandamano kama hayo yalifanyika nchini Marekani karibu na majengo ya Bunge. Pia wafuasi wachache walijitokeza nchini Netherlands kuonesha upinzani wao kwa utawala wa Museveni.

Uganda kwenyewe maandamano ya namna hiyo yalishindwa kufua dafu baada vikosi vya usalama kusambazwa punde tu Bobi Wine alipotangaza maandamano ya amani nchi nzima Machi 2021.

Bobi Wine bado anautuhumu utawala wa Museveni kwa kutekeleza vitendo vya utekaji na mauaji ya wafuasi wake hadi sasa. Ameutaka utawala wa Museveni uache utekaji, iwaachilie huru wafungwa wa kisiasa na kuacha kuwashitaki raia katika mahakama za kijeshi.

Bobi Wine

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Japo Bobi Wine alionekana kuvutia vijana wengi upande wake, mbio zake za kutaka kumtoa madarakani Museveni zimekwama.

Ripoti ya kila mwaka ya World Justice Project (WJP), iliotoka Aprili mwaka huu, inaonesha Uganda ni taifa lenye rikodi mbaya zaidi katika Afrika Mashariki panapohusika utawala wa kisheria.

Ripoti imeiweka Uganda katika nafasi ya 117 duniani kati ya nchi 128 na ya mwisho kwa mataifa ya Afrika Mashariki. Mambo yanayoangaziwa na ripoti hiyo kwa uchache ni haki za kiraia, usalama na uhuru wa kufanya siasa.

Kwa muda mrefu taifa la Uganda chini ya Museveni limekwama kwenye demokrasia yake. Kuna kasoro nyingi. Matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binaadamu, kukandamizwa uhuru wa habari na uhuru wa kufanya siasa yametokea katika kipindi cha uchaguzi.

Shirika linalopambana kumaliza umasikini duniani la Opportunity International, linakadiria 41% ya idadi jumla ya Waganda wanaishi katika umasikini. Huku nusu ya watu wake wakiwa ni watoto chini ya umri miaka 15.

Ufisadi, umasikini, ukosefu wa ajira, bado ni matatizo yanayoiandama Uganda. Uchumi wa nchi hauwezi kusonga mbele pakiwa na ufisadi. Ajira haziwezi kupatikana na umasikini hauwezi kuondoka ikiwa uchumi wa nchi imekwama.

Kwa miaka 35 madarakani, utawala wake haujafanikiwa vizuri katika eneo la uchumi. Miaka yake mitano ijayo hayatazamiwi kuwa na mabadiliko makubwa. Yumkini hali itaendelea kubaki kama ilivyo.


Mataifa mengi ya Afrika yale yenye amani, yako katika vita vya uchumi na demokrasia. Kwa Afrika Mashariki taifa la Kenya linatazamwa kama mfano wa kuigwa kwa demokrasia yake, lakini Wakenya wanalalamika na umasikini na ufisadi.

Taifa la Rwanda linatazamwa kama mfano wa kuigwa katika juhudi zake za kupamba na ufisadi na kuleta mageuzi ya kiuchumi. Ila linakosolewa sana katika demokrasia yake. Siyo sehemu salama kwa wapinzani wa kisiasa wa Rais Paul Kagame.

Taifa la Uganda limekwama katika pande zote mbili. Demokrasia yake ipo katika kiza kinene. Ukuaji wake wa uchumi ni wa mwendo wa kobe. Na bado Yoweri Musevini ana miaka mengine mitano kutawala.

Kuna uhakika kwamba Uganda itaendelea kuwa na amani chini ya Museveni, amedhihirisha hilo liko ndani ya uwezo wake. Ingawa miaka hiyo mitano haijaanza na nyota njema ya kuashiria kuimarika kwa demokrasia ya nchi na kukwamuka katika umasikini uliokithiri.

No comments