simba

CHANZO CHA PICHA,GOAL

Jumamosi, Mei 8, mechi ya soka ya watani wa jadi Tanzania, Simba na Yanga itachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ikiwa ni ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania msimu huu kuanzia saa 11 jioni.

Mechi hiyo itachezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa atakayesaidiwa na Frank Komba, Hamdani Said na Ramadhan Kayoko.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1 ambapo lile la Yanga lilipachikwa na mshambuliaji raia wa Ghana, Michael Sarpong wakati upande wa Simba bao lao lilipachikwa na beki Mkenya, Joash Onyango.

Tofauti na mechi ya mzunguko wa kwanza, Simba na Yanga zinakutana awamu hii katika pambano ambalo lina nafasi kubwa ya kuamua nafasi ya kila timu katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

simba

CHANZO CHA PICHA,SIMBA SPORTS CLUB

Simba inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 61, ushindi katika mechi hii dhidi ya Yanga, utawaweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu ambao utakuwa wa nne mfululizo kwao baada ya kufanya hivyo katika misimu ya 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020.

Kama itapata ushindi, Simba itafikisha jumla ya pointi 64 ambazo zitakuwa ni alama saba zaidi ya zile za Yanga. Mabingwa hao watetezi watakuwa na faida zaidi kwani wamecheza idadi ya mechi mbili pungufu hivyo ikiwa hizo nazo watashinda, maana yake watakuwa juu ya Yanga kwa tofauti ya pointi 13.

Hali ikiwa hivyo, Simba watahitajika kupata ushindi katika mechi mbili tu kati ya sita watakazobakiza ili wajihakikishie kutwaa ubingwa huo.

kk

CHANZO CHA PICHA,YANGA SPORTS CLUB

Lakini kwa Yanga, ushindi katika mechi hiyo, utawasaidia kuwapunguza kasi Simba kwenye mbio za ubingwa, kwani watabakisha pointi moja tu kuwafikia na watabaki kuombea watani wao wapoteze mechi mbili za viporo ili pengo la pointi baina yao lisiwe kubwa.

Matumaini ya Yanga kuinyima Simba fursa ya kutwaa ubingwa msimu huu ikiwa itashinda mechi hii, yanaletwa na uwepo wa baadhi ya mechi ambazo zinaonekana zinaweza kuwa ngumu kwa Simba ambazo mbili ni dhidi ya timu ya Namungo na pia mojamoja itakazocheza dhidi ya Azam FC,Polisi Tanzania na KMC.

Vita ya rekodi

Ni mechi ambayo kila upande na wachezaji mbali ya kusaka pointi za kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa, itanogesha na kiu ama ya kufikia au kuvunja rekodi mbalimbali zilizowahi kuwekwa katika mechi baina ya timu hizo miaka ya nyuma.

Miongoni mwa rekodi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisakwa ni ile iliyowekwa na mshambuliaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, Julai 19, 1977 alipofunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja, ambayo hadi leo hakuna mchezaji mwingine yeyote aliyewahi kufanya hivyo.

Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 6-0, Kibadeni alifunga mabao hayo katika dakika za 10, 42 na 89 huku mengine yakipachikwa na beki wa Yanga, Suleiman Sanga aliyejifunga na Jumanne Hassan 'Masimenti' aliyepachika mabao mawili katika mchezo huo.

Kwa upande mwingine, Yanga watakuwa na kiu ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya Simba ambapo katika mechi 105 walizokutana imeibuka na ushindi mara 37, Simba wakishinda mara 31 na wakitoka sare mara 37. Yanga imefunga mabao 11 na Simba imepachika mabao 100.

Fedha, ustaa vyakoleza joto

Ni mechi ambayo hugeuka neema kwa wachezaji pindi timu husika inapofanya vizuri kutokana na bonasi na zawadi ambazo hupata kutoka kwa viongozi na mashabiki wao lakini pia kwa wachezajin huwa ni fursa kwao kujijengea umaarufu na kuteka hisia za mashabiki na wapenzi wa klabu hizo.

Mara kwa mara wachezaji ambao hufanya vizuri ama kwa kufunga au kucheza kwa kiwango bora katika mechi hizo, hugeuka kuwa lulu na vipenzi vya mamilioni ya mashabiki wa Simba na Yanga.