Breaking News

Njia rahisi ya kuacha kazi na kuanzisha Biashara binafsi

 


 

Katika ulimwengu wa leo karibu kila mwajiriwa ana biashara nje ya kazi ya ajira au anafikiria kuanzisha biashara. Hii inamaanisha kuwa kuna fursa kubwa ya kujipatia kipato cha ziada au hata cha msingi toka katika biashara kama si hivyo watu wasingekimbilia kufanya biashara.

Kuna watu wanaofanya biashara kwa kuwa ndio njia pekee waliyonayo ya kujipatia kipato na kuendesha maisha zao, lakini kwa wale waliojiriwa biashara ni njia mbadala.

Kuna falsafa zinazosema kuwa huwezi kuwa tajiri au kufanikiwa sana kifedha kupitia ajira labda kama utakuwa na nafasi kubwa sana katika kampuni au serikalini na huenda kuna ukweli katika falsafa hii.

Angalia watu waliofanya kwa uadilifu kazi za ajira maisha yao yote na utaona wengi ni masikini sana au wanamudu mahitaji muhimu tu kama chakula , mavazi na malazi.

Hata wale walio makazini hadi leo wanaishi katika maisha ya chini hadi ya kati. Wanaishi kwa kuhesabu siku kusubiria malipo ya mshahara ambao unakutana na mahitaji lukuki yakisubiri na kupotelea huko. Wachache sana wanaweza kutimiza mahitaji yao yote ya muhimu na kubakiwa na kiasi cha ziada kwajiri ya maendeleo yao binafsi na familia zao.

Biashara ina nafasi kubwa zaidi ya kukupa kipato kuliko Ajira
Waajiriwa wanalipa kodi zaidi kuliko wafanya biashara sababu ni kuwa ni rahisi kuwapata na kuwabana. Lakini hata sheria za nchi nyingi duniani zinatoa upendeleo mkubwa kwa wafanyabiashara kuliko wafanya kazi.

Wakati wafanyakazi wanakatwa kodi ya mapato kabla ya matumizi wafanyabiashara wanakatwa kodi baada ya kutoa matumizi waliyofanya na kukatwa kodi katika salio.

Wafanyabishara wajanja wanahakikisha tu kuwa wanaongeza matumizi mengi hata yasiyo ya lazima ili tu faida ionekane kuwa ndogo na hivyo kulipa kodi kidogo.

Wafanyakazi hawana jinsi ya kukwepa kodi na wanalipa kodi mara mbili, Wakisha katwa kodi ya mapato wanakatwa tena kila wanapotumia kununua bidhaa (Kodi ya ongezeko la thamani VAT -18%,Umeme,Mafuta ya Taa,Mafuta ya Magari ,a Gesi ya Kupikia n.k)

Tumia mshahara wa Ajira kama mtaji wa Biashara
Kuanzisha biashara ni suluhisho la kifedha kwa kila mmoja hasa ukiangalia mfumo wa kodi na ushuru wa nchi nyingi duniani kote. Lakini kuanzisha biashara yenye mafanikio kuna changamoto nyingi hasa ukizingatia kuwa matokeo ya tafiti yanaonyesha kuwa katika biashara kumi (10) zinazoanzishwa ni moja (1) tu ndiyo inayohimili kufikia miaka mitano na nyingine tisa(9) zinakufa.

Sababu za kushindwa kwa biashara nyingi kunachangiwa na elimu ndogo ya biashara, mitaji midogo ambayo haitoshelezi kuanzisha biashara yenye kuhimili ushindani na sababu nyingine nyingi.

Hivyo waajiriwa wana nafasi ya kuanzisha biashara kwa kuwekeza toka katika mishahara yao au kuomba mikopo toka tasisi za fedha kama Benki na Vikundi vya Kuweka na Kukopa kwa dhamana ya ajira zao.

Fedha hizi zikiwekezwa vizuri katika biashara iliyopangwa vizuri itaweza kulipa deni na kuweza kumlipa muwekezaji na hivyo kuwa chanzo cha pili cha kipato.

Mwajiriwa anaweza akaanzisha biashara nyingi kutumia mbinu hii hivyo kuwa na vipato toka vyanzo vingi kitu ambacho kitamfanya awe na mafanikio makubwa kifedha.

Pata Elimu ya Bishara kabla ya kuanza
Jifunze namna ya kufanya biashara kwanza,watu wanaanza biashara na kutegemea kufanikiwa lakini wanasahau kuwa ili kufanikiwa katika chochote ni lazima uwe na weledi wa kutosha katika jambo hilo. Elimu ya biashara ni muhimu ili kupata mafanikio katika kuanzisha na kuendesha biashara kwa mafanikio.

Unaweza kupata elimu toka kwa wafanyabiashara wazoefu na waliofanikiwa tayari au kwa kujiunga na kozi fupi ya ujasiriamali au semina mbalimbali za biashara.

Fanya utafiti wa mahitaji na masoko ya bidhaa au huduma unazotaka kutoa
Kuanzisha biashara inayouza bidhaa ambazo hazina uhitaji mkubwa ni makosa yanayofanywa na wengi. Tunaanzisha biashara na kutegemea watu waje kununua bila kufanya utafiti wa kutosha kujua kama bidhaa au huduma zako zinahitajika.

Hakikisha unafanya utafiti wa kutosha. Biashara yako itakuwa rahisi kuuza kama bidhaa na huduma unazotoa zinahitajika na zinasaidia watu kutatua matatizo yao.

Mfano: Bishara ya usafiri wa Watoto wa Shule
Kutoa huduma ya usafiri salama na uhakika kwa wanafunzi kwenda na kurudi toka shuleni. Huduma hii inahitajika sehemu nyingi na wazazi wanapata shida kuwapeleka watoto shuleni na wenyewe kuwahi kazini.

Kama utaweza kuwa na gari zuri ambalo watoto wote watakaa katika viti na una kiyoyozi ndani ili watoto wasipate vumbi unaweza ukaanzisha huduma hii na ni rahisi kupata wateja kwa sababu wazazi wanataka usalama wa watoto wao na wako tayari kulipa kwa huduma nzuri.

Ajiri mtu mwenye Ujuzi
Wataalamu wanasema kuwa ili iitwe biashara ni muhimu kutengeneza mfumo ambao utafanya kazi ukiwepo au usiwepo lasivyo hiyo ni ajira binafsi. Biashara inatakiwa iendelee hata kama umelala nyumbani au umesafiri.

Kwa misingi hii basi kwa kuwa wewe ni mwajiriwa bado hutapata muda wa kusimamia muda wote hivyo utatakiwa kuajiri mtu ambaye ataendesha. Ni vizuri mtu huyu akawa na elimu ya masoko na huduma kwa wateja ambayo ni muhimu sana kwa biashara yoyote


Tunza mahesabu ya Biashara kwa usahihi
Hakikisha mahesabu yote ya manunuzi,mauzo na malipo yanatunzwa kwa usahihi kwaajili ya kupata taarifa za maedeleo ya biashara yako.

Fungua akaunti maalumu ya benki kwa ajiri ya biashara pekee.

Jilipe Mwenyewe Mshahara
Dhumuni a kuanzisha biashara ni kuongeza chanzo cha mapato binafsi. Hivyo hakikisha unaweka kiasi fulani cha fedha na ujilipe na hesabu kama ni matumizi ya biashara. Unaweza ukajilipa toka katika faida unayotengeneza kama asilimia au kiasi maalumu. Fanya hivyo kwa biashara zote kama unayo zaidi ya moja.

Je ni wakati gani ni muafaka kuacha kazi?
Endelea kufuatilia vipato vyako toka biashara zako zote. Ni vizuri kuwa na biashara angalau mbili kwa usalama zaidi.

Mapato yako yatokanayo na biashara yanapokuwa sawa au zaidi ya mshahara wa ajira ni muda sahihi na salama kuacha kazi na kujihusisha muda wote na kusimamia na kuendesha biashara zako.

Utakapoacha kazi utapata muda mwingi zaidi wa kusimamia biashara zako na hivyo kuongeza ufanisi.

Mafao utakayoyapata baada ya kuacha kazi unaweza ukaanzisha biashara nyingine au kuongezea mtaji katika biashara ulizo nazo tayari.

Hii ni njia sahihi na salama kuacha kazi na kuanzisha biashara binafsi.

Je wewe una mpango gani kuhusu kuanzisha biashara binafsi na kuacha kazi ya ajira? Nini mtazamo wako kuhusu mpango huu wa kuacha kazi na kuanzisha biashara binafsi?

Asante kwa kusoma na nawatakieni mafanikio mema.

No comments