Breaking News

Kaizer Chief inavyotishia ndoto za Simba kuvunja rekodi ya 1974

 


simba

CHANZO CHA PICHA,SIMBA-TWITTER

Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu imechezeshwa juzi huko Cairo, Misri ambapo timu nne zilizoongoza katika hatua ya makundi zimejua klabu zitakazokabiliana nazo katika hatua hiyo.

Kwa mujibu wa droo hiyo, Simba ya Tanzania iliyoongoza kundi A imepangwa kukutana na washindi wa pili wa kundi C, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini wakati Al Ahly ya Misri itacheza dhidi ya Mamelodi Sundowns iliyoongoza kundi B.

Vinara wa kundi C, Wydad Casablanca ya Morocco wenyewe watacheza na MC Alger ya Algeria wakati huo timu ya Esperance ya Tunisia itakabiliana na CR Belouizdad ya Algeria.

Ratiba ya robo fainali inaonyesha kwamba mechi za kwanza za hatua hiyo zitachezwa kati ya Mei 14 na 15 ambapo timu zilizoshika nafasi ya pili katika hatua ya makundi zitaanzia nyumbani na michezo ya marudiano imepangwa kuchezwa kati ya Mei 21 na 22.

Nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla, matumaini yamekuwa makubwa kwa Simba kwamba itaweza kupata matokeo mazuri dhidi ya Kaizer Chiefs na kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo na pengine hata kufuzu fainali au kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Ziko sababu mbalimbali ambazo zinawapa mashabiki wengi wa soka Tanzania na Afrika Mashariki kiujumla imani kwamba Simba itaweza kupenya mbele ya Kaizer Chiefs licha ya heshima kubwa ambayo wapinzani wao hao wanayo katika soka la Afrika na Afrika Kusini kiujumla.

Kaizer Chiefs

CHANZO CHA PICHA,TWITTER

Mojawapo ya sababu hizo ni kiwango bora kilichoonyeshwa na Simba katika hatua ya makundi ambapo ilionekana kuwa imara na kukamilika katika kila idara kuanzia ile ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji kulinganisha na Kaizer Chiefs ambayo haikutamba sana katika hatua hiyo.

Simba licha ya kuongoza kundi lake ikiwa na pointi 13, ilikuwa miongoni mwa timu zilizofunga idadi kubwa ya mabao ikipachika mabao tisa lakini ilishika nafasi ya pili kwa kuwa na safu imara ya ulinzi katika hatua ya makundi ikifungwa mabao mawili tu tofauti na Kaizer Chiefs ambayo ilimaliza ikiwa nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi tisa kwenye kundi lake, ikifunga mabao matano na kufungwa jumla ya mabao sita.

Lakini pia kiwango cha mchezaji mmojammoja kilichoonyeshwa na nyota wa Simba ni sababu nyingine inayowafanya wengi waipe nafasi ya kwanza Simba kupata matokeo mazuri mbele ya Kaizer Chiefs ambayo idadi kubwa ya wachezaji wake hawkauwa na muendelezo mzuri wa ubora kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Kipa Aishi Manula ni miongoni mwa walinda mlango bora watano ambao walicheza idadi kubwa ya mechi za makundi bila kuruhusu bao akifanya hivyo katika mechi tatu, mshambuliaji Luis Miquissone akiwa kinara wa kufumania nyavu akipachika mabao matatu huku kiungo Clatous Chama akiwa kinara wa kupiga pasi zilizozaa mabao akiwa nazo tatu sawa na Themba Zwane wa Mamelodi.


Ikiwa Simba itaitupa nje Kaizer Chiefs na ikafanikiwa kutinga hatua ya fainali kama pia itapenya katika nusu fainali, itakuwa imevunja rekodi yake ya mwaka 1974 ambapo waliishia katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwaka 1974, Simba ilikomea katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penati 3-0 ugenini huko Misri na timu ya Mehalla El Kubra kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi mbili baina yao.

Simba ilianza kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani na ilipoenda ugenini ikafungwa kwa matokeo kama hayo ndipo ikaamriwa mshindi apatikane kwa mikwaju ya penati na hapo Simba wakajikuta wakikwama.

Kabla ya kukutana na Mehalla, Simba ilianza kwa kuitupa nje timu ya Linare kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 na hatua iliyofuata wakaitoa Green Buffaloes ya Zambia kwa mabao 3-1 na robo fainali wakaifunga Hearts of Oak ya Ghana kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1

Lakini kiuhalisia kama Simba wasipojipanga vyema, ndoto ya kufika fainali ama kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu inaweza kukomea kwa Kaizer Chiefs na ziko sababu kadhaa zinazoweza kupelekea hilo

Ubabe wa Kaizer Chiefs ugenini

Timu ambazo zimekuwa na uwezo wa kupata matokeo mazuri ugenini huwa na nafasi kubwa ya kufanya vyema katika mashindano ya klabu barani Afrika na Kaizer Chiefs msimu huu wameonyesha wanamudu kufanya hivyo.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Kaizer Chiefs wamecheza jumla ya mechi tano ugenini ambapo kati ya hizo wamepata ushindi katika michezo miwili, wametoka sare mbili na kupoteza mechi moja, wakifunga mabao manne na kufungwa mabao sita.

Hii ni tofauti na Simba ambao katika mechi tano za ugenini, wamepata ushindi mara mbili, wametoka sare moja na kupoteza mechi moja, wakifunga mabao mawili na kufungwa mabao mawili.

Ubora wa wachezaji

Kaizer Chiefs inaundwa na kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo binafsi na walio na uzoefu wa kucheza mechi za mashindano makubwa kulinganisha na Simba jambo linaloweza kuwapa faida timu hiyo ya Afrika Kusini.

Kipa na nahodha wao Itumeleng Khune alikuwemo katika kikosi cha Afrika Kusini kilichocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 kama ilivyo kwa mshambuliaji Bernard Parker wakati huo kipa msaidizi, Daniel Akpey alikuwemo katika kikosi cha Nigeria kilichocheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 kule Brazil.

Pia wana idadi kubwa ya nyota kutoka mataifa nguli ya soka Afrika na duniani kwa ujumla mfano ni Willard Katsande na Khama Billiat (Zimbabwe), David Castro (Colombia) na Samir Nurkovic kutoka Serbia.

Uzoefu wa kocha

Kaizer Chiefs

CHANZO CHA PICHA,TWITTER- KAIZER CHIEFS

Kocha wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt ni aina ya wakufunzi ambao wamekuwa wakizimudu mechi za presha na zile za mtoano na ndio maana sio jambo la ajabu kuona akiwa ametwaa idadi kubwa ya mataji katika timu alizofundisha kulinganisha na mwenzake wa Simba, Didier Gomes Da Rosa.

Wakati Didier Gomes Da Rosa akiwa ametwaa mataji sita tu katika timu zote aliwazowahi kufundisha, kocha Gavin Hunt wa Kaizer Chiefs yeye ametwaa jumla ya mataji saba.

Ratiba ngumu ya Simba

SIMBA

CHANZO CHA PICHA,TWITTER-SIMBA

Siku chache kabla ya mchezo wao wa kwanza ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs, Simba watakabiliwa na mchezo mgumu wa watani wa jadi dhidi ya yanga, Mei 8 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hii maana yake ni kwamba, Simba watakuwa na muda mchache wa maandalizi kabla ya kuvaana na Kaizer Chiefs, lakini kabla ya mechi ya marudiano, Simba watakabiliwa na mechi za viporo vya Ligi Kuu ambazo bado hazijapangiwa tarehe.

No comments