Wapi ilipo kete yake muhimu kisiasa?
Samia ndiye atakuwa mwanamke wa kwanza katika historia kuwa Mwenyekiti wa CCM. Tafiti nyingi za ndani za CCM zimekuwa zikionyesha kwamba bado kinaungwa mkono na wanawake katika makundi tofauti na hili ni eneo ambalo huenda akalitumia vizuri.
Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, timu ya kampeni ya Samia aliyekuwa mgombea mwenza iliundwa pia na wanawake wengi vijana na alitengeneza nao uhusiano uliofanya awe anaalikwa katika matukio mengi ya akinamama - ikiwamo Siku ya Wanawake Duniani alikoalikwa kuwa mgeni rasmi mwaka huu.
Katika hotuba yake bungeni, Samia alitamka hadharani kwamba katika mambo yake yote ya kisiasa, jambo lililo karibu zaidi na moyo wake ni lile la kuzuia vifo vya wanawake wajawazito na watoto.
Kuna sababu zote kuamini kwamba Samia atajitahidi kuifanya CCM iwe rafiki na karibu kwa wanawake, jambo ambalo litakuwa na faida ya kukizimua chama chake na kuingiza wanachama wapya ambao pengine bila juhudi za makusudi za kusaidia wanawake, wasingeweza kujiunga.
Kundi hili la wanawake litagusa pia kundi la jumla la vijana na tayari Samia ameshaonyesha kulifahamu kwa kuzungumza misemo kama "Ukizingua nami nakuzingua" ambao kundi la vijana linaweza kujihusisha nalo.
Kauli zake za mwanzo kama Rais zinamwonesha kama Mwenyekiti atakayekuwa karibu na biashara na wawekezaji - na kama eneo hilo litafanya vizuri, anaweza kujikuta akisaidia katika kupambana na tatizo la ajira linaloathiri vijana wengi hapa nchini.
No comments