Fahamu mambo yatakayojadiliwa baina ya Rais Samia na wapinzani Tanzania
Katika hali ya kawaida upinzani na upande wa chama tawala hukutana katika sanduku la kura au majengo ya kutunga sheria.
Ila panapokuwa na vikao vya faragha, vyenye lengo la kuletea suluhu kati ya pande hizo mbili, tafsiri yake ni kuwa mfumo uliopo unaoendesha siasa una walakini.
Tangu Tanzania ianze kuwa na chaguzi za vyama vingi, mara nyingi misigano kati ya utawala na vyama vya upinzani ilishika kasi wakati ule wa kuelekea uchaguzi mkuu au baada ya uchaguzi huo kuisha. Kulikuwa na nyakati za ahueni na ukimya wa kisiasa.
Katika utawala wa hayati John Pombe Magufuli misigano ya kisiasa kati ya utawala wake na upinzani haikuwa ya msimu tena. Ilianza tu alipoingia madarakani na iliendelea hadi siku alipofariki dunia. Hali hiyo ilichagizwa na sera zake zinazokosoloewa kuwa ni za kikandamizaji.
Rais mpya, Samia Suluhu Hassan anaoneka kutaka kuondoa misigano hiyo. Aprili 22, akitoa hotuba yake ya kwanza iliyotoa dira ya serikali yake ndani ya Bunge jinini Dodoma, alieleza azma yake ya kutaka kuonana na vyama vya kisiasa.
Kabla ya Rais Samia kueleza hilo, Aprili 11, 2021, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alieleza kuwa chama hicho kiliandika barua kutaka kuonana na Rais Samia. Kwa maana hiyo ombi lao limekubaliwa.
Baada ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Rais wa Tanzania wa wakati huo, John Magufuli alikiri kupokea barua tatu kutoka kwa Maalim baada ya mkwamo wa 2015 uliotokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huovisiwani Zanzibar.
Hadi Machi 2020, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, Watanzania ndipo waliposhuhudia viongozi hao wakikutana kwa kikao cha faragha; Maalim alialikwa na Magufuli katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam.
Msururu wa vikao vya Magufuli na viongozi wa upinzani, haukushirikisha kiongozi yeyote wa Chama kikuu cha upinzani Chadema. Lakini Rais Samia ameweka wazi kukutana na vyama vya kisiasa. Hii ina maana vyama vilivyo hai vitapata wasaa wa kuzungumza naye.
Tume huru ya uchaguzi
Mjadala wa tume huru, huenda ukaanza katika katiba mpya. Upinzani utakuwa na hamu ya kuona Tanzania ikiwa na katiba mpya ili itatue baadhi ya changamoto katika mifumo ya siasa za sasa.
Hoja ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi, huenda ikaleta mabishano kwa sababu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), tume huru haipewi kipaumbele.
Kwani mfumo wa sasa wa tume hiyo huonekana kuegemea upande wa chama tawala. Hii ina maana chama chochote kitakachokuwa madarakani, muundo wa tume ya sasa unawapa nafuu.
Ikiwa Mama Samia atadhamiria kubadili muundo wa tume ili iwe huru, atakuwa na kazi ya ziada ya kupambana na upinzani wa wazi au usio wa wazi utakao zuka kutoka kwa wakereketwa wa chama tawala.
Uhuru wa vyombo ya habari
Kwa miaka mingi vyombo vya habari vyenye mrengo wa upinzani au vile visivyoogopa kuikosoa serikali, vilikuwa ni jukwaa muhimu kwa vyama hivyo kupaza sauti zao. Kwa namna ya kukosoa utawala na kupigia chapuo upande wao.
Asilimia kubwa ya vyombo hivyo aidha vilipigwa maonyo, vilifungiwa kwa muda au kupigwa marufuku kabisa katika utawala wa hayati Magufuli. Mfano wa yaliyofungiwa kabasa ni gazeti la MwanaHalisi, Mawio, Tanzania Daima na Mseto.
Licha ya Rais Samia kuamuru runinga za mtandaoni kurudi hewani zile ambazo zilifungiwa, bado magazeti yamewekwa pembeni katika amri hiyo.
Uhuru wa habari hauhusiani pekee na kuvitoa kifungoni vyombo vilivyofungiwa. Pia, una mlahaka na vyombo hivyo kuandika na kuripoti bila ya kubughudhiwa na utawala.
Miaka mitano ya hayati Magufuli kulishuhudiwa vyombo kadhaa vikipigwa faini, kufungiwa, vikipewa adhabu na kulikosekana ule uhuru wa kuikosoa serikali na ukajihisi uko katika amani.
Uhuru wa kisiasa
Moja ya mjadala utakao kuwa mtihani mkubwa kwa pande zote mbili, ni uhuru wa kisiasa. Utawala uliopita ulipiga marufuku mambo makubwa mawili; maandamano na mikutano ya hadhara. Isipokuwa kila Mbunge akafanye mkutano katika jimbo lake.
Rais Samia atakuwa na uwezo wa moja kwa moja kuwahakikishia usalama viongozi wa upinzani, kwamba hakuna Polisi atakae wavamia kama ilivyokuwa katika mikutano yao ya ndani na wala hakutokuwa na watu watakao tishia ama kuandaa majaribio ya kuwahuru au hata kuwauwa pindi wakikosoa utawala.
Fauka ya hilo, atakuwa na uwezo wa kuwahakikishia usalama wanasiasa waliokimbia nje ya Tanzania, akiwemo Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Wanaweza kurudi na hakuna baya litawapata.
Lililo gumu ni hili: Je, atakubali vyama vya upinzani vifanye maandamano na kuzungunka nchi nzima kufanya mikutano?
Hili ni swali gumu, kwa sababu marufuku ya sasa ni ahueni kisiasa kwa chama tawala. Na CCM inapendelea marufuku hii iendelee kuwepo kwa faida yake.
Kwa upande mwingine, ikiwa vyama vya upinzani vitakubali uwepo wao bila ya kuendesha maandamano na mikutano mikubwa ya kisiasa, huu utakuwa ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika siasa za Tanzania. Kwamba upinzani umekubali hakuna tena shughuli za nje za kisiasa hadi unapokaribia uchaguzi mkuu.
Mazungumzo haya yana umuhimu gani?
Sura ya Tanzania kimataifa sio nzuri panapohusika uhuru wa kisiasa na uhuru wa habari. Utawala uliopita uliendesha kampeni za makusudi zilizoathiri siasa na shughuli za vyombo vya habari.
Mazungumzo haya ni muhimu kwa muktadha wa kuisafisha sura ya nchi ndani na nje nje ya mipaka. Tanzania ilifika kujadiliwa kuwekewa vikwazo na mataifa makubwa kwa kuzorota demokrasia yake.
Pia Rais Samia anafungua ukurasa mpya baada ya mahusiano yaliyodorora ya utawala na upinzani. Kwa mtawala yeyote uhusiano mwema na upinzani ni bora kuliko uhusiano wenye mashaka.
Kufanyika kwa mkutano huu bila ya kujali matokeo ya mkutano wenyewe ni mwanzo mpya kwa siasa za nchi. Mikutano ya namna hii iliisha wakati wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Wakati huo vyama vya upinzani vilifanya shughuli zao, hadi Chadema kuitwa, 'chama cha maandamano,' na wakosoaji wake. Walitumia haki yao ya kuandamana, kukosoa na kufanya mikutano kiasi cha kuitia tumbo joto serikali hadi kuitwa Ikulu.
Kwa Magufuli aliona huo ni udhaifu na usumbufu, ndio maana milango ya maandamano na mikutano akaifunga. Alifanikiwa kudhibiti siasa za upinzani, kwa upande mwingine aliharibu kabisa sura ya utawala wake hadi kulifikisha jina lake katika mjadala wa udikteta.
Rais Samia hatotaka jina lake lifike katika mjadala wa aina hiyo. Pia, yawezekana hatotaka utawala wake utikiswe asubuhi na mchana na upinzani kama ilivyokuwa kwa Kikwete. Kwa kuzingatia hayo, mazungumzo yake na wapinzani ni kikao chenye mtihani mkubwa kwake.
Kikao kitaamua ikiwa kauli yake; yeye na hayati Magufuli walikuwa kitu kimoja. Je, anamaanisha kwa yale mazuri tu au hata yale yenye kuleta sura mbaya kwa afya ya demokrasia ya nchi?.
No comments