Breaking News

CCM inayobebwa na dola, isiyopendwa na vijana


Samia anakabidhiwa Uenyekiti wa CCM miezi michache tu baada ya chama chake kuibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu unaoelezwa kuwa "usiokuwa wa kidemokrasia' kuliko mwingine wowote katika historia ya chaguzi za vyama vingi hapa nchini.

CCM iliibuka na ushindi - Tanzania na Zanzibar, mbele ya malalamiko ya wapinzani kukatwa majina, wingi wa kura bandia, viongozi wa upinzani kushambuliwa na wengine kukimbilia nje ya nchi na tuhuma za wagombea wa upinzani kushawishiwa au kutishwa kujiunga na chama tawala.

Zanzibar, anakotoka Samia, aliyekuwa mgombea wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, hayati Seif Shariff Hamad, alipata chini ya asilimia 20 ya kura zote zilizopigwa - jambo ambalo wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar hawalioni kama linawezekana kwa muktadha wa siasa za huko.

Ingawa kuna wasioitaka CCM kwa sababu tu kimekaa madarakani muda mrefu na wangetamani mabadiliko; kiu ya kawaida ya mwanadamu, baadhi ya vitendo vilivyotokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, vimewatia sababu nyingine zaidi ya kutaka CCM iondoke.

Samia anarithi CCM ambayo vijana wengi hawataki kuhusishwa nayo - ingawa wanatengeneza zaidi ya nusu ya wapiga kura wote, iliyogawanywa na siasa za minyukano za takribani miaka 20 sasa na inayohitaji kujitenganisha na dola ili ionekane inasimama kama chama cha siasa.

Minyukano ndani ya CCM ilianza tangu wakati wa Mkapa lakini ilichochewa zaidi wakati wa Kikwete ambako ilifikia wakati chama kikataka kujivua gamba na kuibua mgogoro ambao hatma yake ilikuwa kwa wana CCM kuimba hadharani kuwa wana imani na mtu asiyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho.

Minyukano hiyo iliendelea wakati wa Uenyekiti wa Magufuli, ambaye ni kama alitaka kutengeneza kilichoanza kuitwa CCM Mpya - akiachana na watu waliofahamika kama wana CCM kindakindaki na kuchukua wanachama kutoka vyama vya upinzani na watu wengine walioonekana kama wageni kwenye chama.

Wakati Magufuli anafariki dunia, aliyekuwa Katibu Mkuu wake wa mwisho, Dk. Bashiru Ally na Katibu Mwenezi, Humphrey Polepole, walikuwa hawajawahi kuwania nafasi yoyote ya kiuchaguzi katika ngazi za juu za CCM kabla hawajateuliwa kushika nyadhifa zao hizo.

Kama Magufuli angeendelea na uongozi wake mpaka mwisho, kulikuwa na uwezekano kuwa CCM hii ya sasa kama inavyoonekana, ingekuwa na mwonekano tofauti na viongozi na vinara wake wangekuwa watu ambao hawajazoeleka sana machoni na masikioni mwa Watanzania.

Magufuli alichaguliwa kuwa Mwenyekiti akiwa hajawahi kuwa hata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na pengine tabia yake hiyo kama kiongozi wa chama iliakisi historia yake ya nyuma kama mtu asiye kada wa chama na asiye na fungamano na chama hicho. Kwa kawaida, CCM huakisi taswira ya Mwenyekiti wake.

No comments